Baada ya kuwaletea makala kuhusu Historia, Maana na asili ya jina Mbulu na pia Taratibu za kufuata kama unataka kuoa Mwiraqw, kuanzia leo nitakuwa nawaletea kuhusu jamii au kabila la Wadatooga.
Nikiwa katika harakati za kutengeneza filamu kuhusu Historia, Maisha na Hatma yao kama jamii ambayo imepewa jina la Datooga:Geeleabu yeenu ak ghamneawa geendi yeenu? Ak geegalli yeenu? nimeona niwaletee wasomaji wangu waweze kujifunza mambo mawili matatu kuhusu Wadatoda.
Je Wadatooga ni watu gani?
Wadatooga au watatooga kama wanavyoitwa ni jamii ya kinailotiki wa nyanda za juu ambao wanapatikana Kaskazini mwa Tanzania hasa katika wilaya za Mbulu na Hanang mkoani Manyara japo katika miaka ya hivi karibuni wamesambaa nchi nzima ya Tanzania kusaka malisho ya mifugo yao. Kuna aina mbili za Wanailotiki ambazo ni Wanailotiki wa Nyanda za juu yaani Highland(Southern) Nilotics ambao ni jamii za Wadatooga wa Tanzania, Dorobo na Kalenjin wa Kenya na Wanailotiki wa nyanda tambarare yaani Plains Nilotics kama Wamasai na Luo wa Kenya. Kama wanailotiki wengine, wadatooga asili yao ni Sudan na Magharibi mwa Ethiopia na walifuata bonge la mto Nile (ndio maana wanaitwa Nilotes) kuelekea Kusini
Makundi ya Wadatooga (Dialects)
Kuna lahaja (Dialects) ambazo ndizo zinazounda makundi mbalimbali ya Wadatooga. Makundi haya hutofautina katika mambo kadha wa kadha. Makundi haya ni
- Barbayiga (Barbayiiga)
- Gisamajanga
- Bajuta
- Rotigenga
- Burediga
- Hojabooga
- Isimijeega
- Gidang`odiga
- Bisiyega
- Darorajega
- Daregwajega
- Damarga
- Utatu (taturu, Biyenjida)
Wadatooga wote hutambulishwa kwa wanawake wao wanapoolewa kuvalishwa sketi ya ngozi ``Hanang`wenda`` na hujiita ``Geda hanang`wenda`` yaani wavaa ngozi.
Barbayiga (au Barbaig kama wanavyofahamika na wengi) yaani wapiga fimbo au wapenda fimbo kutokana na kupiga fimbo wakati wanacheza ngoma na pia kupenda kukata fimbo kila wanapoona mti unaofaa kwa fimbo ndilo kundi kubwa kuliko yote kwa wadatooga na hivyo kupelekea watu wengi kuwaita wadatooga wote kuwa ni Wabarbayiga.
Historia
Rotigenga wagawanyikia Mlima Elgon
Utafiti unaonesha kuwa walifika mpaka Mlima Elgon uliopo mpakani mwa Kenya na Uganda katika karne ya 18 waligawanyika ambapo Rotigenga waliendelea kuelekea kusini hadi pwani ya mashariki ya ziwa Victoria (wadatooga wanaliita Lahu) na kuishi hapo, mpaka leo hii wapo huko Mara.
Kundi kubwa lililobaki lilielekea kusini mashariki hadi magharibi mwa mlima Kilimantaro (West Kilimanjaro). Mlima ambao wadatooga wanauita Gijedamar yaani ``mtu mwenye kipara, au mlima uliokama shujaa aliyeua Simba`` kutokana na barafu iliyopo juu ya mlima huo kwani wadatooga wanapompongeza mtu kwa ushujaa wake humwekea mafuta ya siagi ya ng`ombe kichwani kama barafu ya Mlima Kilimanjaro ilivyo"
Hapo wakakuta na Wamasai ambao walipigana sana na kuelekea magharibi wakipita Mlima Oldonyo Lengai wanaouita Gijeda Sakuraraig yaani mlima unaotapika moto hadi kreta ya Ngorongoro wanayoiita Fued ambako walikaa kwa miongo mingi sana kabla ya kuondoka hapo baada ya vita na mahasimu wao wakubwa yaani wamasai.
Kutoka Ngorongoro walizidi kusonga kuelekea magharibi hadi bonde la ziwa Eyasi (Mang`ola) ambako wakagawanyika tena ambako kundi moja liliamua kuendelea kuelekea magharibi na kundi lingine likapanda kwenye uwanda wa juu wa bonde la ufa wakielekea kusini magharibi.
Kundi lililoelekea Magharibi
Hili kundi lililoelekea Magharibi lilipofika magharibi mwa ziwa Eyasi maeneo ya Maswa ya sasa, Buradiga wakaamua kubaki pale na ndipo wanapopatikana mpaka leo huku Barbayiga wakiendelea kuelekea Magharibi wakisaka malisho na maji kwa ajili ya mifugo inasemekana wakafika hadi Tabora. Wadattoga wanadai kuwa hata jina la Tabora linaasili yao kwani huko kuna kaburi la mtu moja tajiri sana wa ng`ombe aliyeitwa Bora na kufanyiwa Bung`eda na hivyo kulirefer kama ``Bung`eda Bora) na hatimaye jina hilo kubadilika kuwa Tabora. Hili laweza kuwa kweli kwani majina ya maeneo karibu yote katika maeneo walikopita ni ya Kidatooga hasa katika wilaya za Mbulu na Hanang. (Nitaeleza kuhusu Bung`eda katika sehemu nyingine)
Kutoka Tabora wakaamua kuelekea kusini mashariki hadi Singida na wanadai pia kuwa Singida alikuwa tajiri moja wa Kidatooga aliyekuwa na ng`ombe wengi sana na Bung`eda yake ipo hapo hata sasa. Wakiwa hapo Singida bado waliandamwa na tatizo lile lile la maji kwa ajili ya mifugo yao.
Huko nyuma nako kwa Buradiga, kundi lingine likaamua kuondoka hapo likafika hadi maeneo ya Itigi na kuishi hapo mpaka sasa na hawa ndio Utatu au Biyenjida au Taturu
Kundi lililopanda kwenye uwanda wa juu wa Bonde la Ufa
Kuna waliobaki maeneo ya Mang`ola na maeneo ya ziwa Eyasi wanaloliita Balang`ida Mwamba mfano Isimjega na Daregwajega huku wengine wakipanda hadi maeneo ya Mbulu na kukaa hapo. Gisamjenga walifika Mbulu, Gehandu hadi Dongobesh na wakaishi katika hayo maeneo huku Damarga wakikaa maeneo ya Tlawi ambapo ziwa Tlawi huitwa Basso damarga hata leo.
Dararajega walieendelea hadi wakafika ziwa Bassotu kaskazini magaribi mwa mlima Hanang wakakaa hapo na nyuma yao wakaja Hojabooga ambao walipowakuta Darerajega wanafaidi maji fresh ya ziwa Bassotu ikaibuka vita na Darerajega wengi waliuliwa na Hojabooga kutawala ziwa Bassotu.
Gidang`odiga ambao tofauti na wadatooga wengine, wao si wafugaji bali ni wahunzi wakitengeneza zana mbalimbali na silaha kwa ajili ya makundi mengine. Gidang`odiga maarufu kama Karera wanavyoitwa na Wairaqw wao wapo na wanaishi katikati ya makundi mengine lakini cha ajabu hawaoani na jamii nyingine hasa Barbayiga na Gisamjanga na wapo kwa wingi maeneo ya Dawr, Mewadan na Dongobesh
Barbaig wafika Bassotu
Baada ya kuishi Singida kwa miaka mingi na bado maji yakiwa bado tatizo kubwa kwao, inasemekana kuwa vijana wa Kibarbayiga waligundua uwepo wa ziwa Bassotu wakiwa katika harakati za kumtafuta ng`ombe dume aliyepotea. Uwepo wa maji fresh uliwahamasisha Barbayiga kuhamia Bassotu na ndipo yakatokea mapigano baina yao na Hojabooga na hatimaye Barbayiga kushinda na kutawala maeneo ya Bassotu, kisha kusambaa hadi mlima Hanang upande wa magharibi na kusini.
Bajuta watoka kwa Rotigenga Musoma
Ikumbukwe kuwa Rotigenga walijitenga karne nyingi sana na hawakuwa na mwingiliano wowote na wadatoga wengine bado walikuwa wanajitambulisha kama wadatooga. Baada ya karne nyingi, kundi moja liliondoka huko Musoma kutoka kwa Rotigenga na kupita katikati ya uwanda wa Serengeti hadi Mang`ola. Kundi hili ambalo ndilo Bajuta, ndilo kundi mashuhuri miongoni mwa wadatoga wote kama waganga mashuhuri na hata Nabii ambaye wadatooga wote wanamheshimu na kumuenzi yaani Saigilo Magena (Niteleza kuhusu Saigilo katika mada nyingine) alitokea kwa Bajuta. Bajuta wakaenda mpaka maswa, wakazunguka hadi singida na kisha kuingia Mbulu na kujichanganya na wadatooga wengine.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni