Arts and Culture for Youths Organization, S.L.P 10777 Mwanza - Tanzania. Baruapepe:arcuyo2014@gmail.com,Simu: +255 (0) 767 122910/ 752 512088/ 759 543919/ 658 23140
Jumapili, 1 Novemba 2015
Uchaguzi umekwisha, sasa iwe kazi tu
HATUA ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kumkabidhi cheti mshindi wa kinyang’anyiro cha urais, Dk John Magufuli na mgombea mwenza, Samia Suluhu Hassan, inaashiria kumalizika rasmi kwa mchakato wa uchaguzi mkuu wa Tanzania unaosimamiwa na tume hiyo. Ni kweli katika uchaguzi wowote, kila mgombea huwa na matarajio ya kushinda na wanaomuunga mkono huweka matumaini kwake na hivyo ni jambo la kawaida kwa walioshindwa kuumia.
Maumivu yanaweza kuwa makubwa au mepesi, kutegemea na namna mhusika na wafuasi wake, walivyojiandaa kisaikolojia kupokea matokeo, yawe mabaya au mazuri kwao. Kwa hatua iliyofikiwa, kuendelea kulalamika mitaani kwenye magenge na vijiwe vya kahawa, hakusaidii lolote, isipokuwa la muhimu ni kukubaliana na matokeo na kumshukuru Mungu kwa kuipitisha nchi salama katika uchaguzi na kufungua ukurasa mwingine wa kuendelea na ujenzi wa nchi, kwani baada ya uchaguzi maisha lazima yaendelee.
Kwa ngazi ya ubunge, kama kuna malalamiko na hao wanaolalamika wanadhani wana ushahidi kwamba uchaguzi katika maeneo yao ulivurugwa, kinachotakiwa ni kufuata taratibu zilizopo katika kutafuta haki huku wakiendelea kutoa ushirikiano kwa waliokabidhiwa ofisi za uongozi. Uchaguzi wa mwaka huu, ulijielekeza katika dhana ya mabadiliko.
Bila shaka mabadiliko yanayotarajiwa hapa ni pamoja na wananchi wenyewe kubadilika kwa maana ya kuchapa kazi kwa bidii zaidi ili kupata mafanikio maradufu na siyo kusubiri kufanyiwa kila kitu na viongozi au serikali mithili ya ndege anavyolisha makinda yake.
Ni kwa muktadha huo, tunasema wakati uongozi mpya ukijipanga kutekeleza ahadi zake nyingi walizotoa wakati wa kampeni, kila mwananchi ana dhima kubwa ya kusaidia uongozi mpya kutekeleza kwa urahisi majukumu yake na moja ya dhima hiyo ni kuchapa kazi kwa bidii, maarifa na uadilifu.
Hakuna namna yoyote Watanzania watatazamia kupata mabadiliko, hata kama watawekewa lami hadi vichochoroni, maji na umeme wa kumwaga, huduma za afya na shule kila mtaa, kama watakalia kupiga soga vijiweni na kuendelea kujadili yaliyopita, hususan mchakato wa uchaguzi, badala ya kufanya kazi kwa bidii na kuupa ushirikiano wa kutosha uongozi mpya.
Ni muhimu pia kurejesha umoja na mshikamano kama Watanzania na kuweka maslahi ya nchi mbele kila wakati. Hili linatakiwa liende sambamba na kuwaombea kila la heri na baraka kwa Mwenyezi Mungu viongozi waliochaguliwa, kwani wanaposhindwa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, labda kutokana na kukosa ushirikiano, kila mwananchi bila kujali itikadi yake ya kisiasa, dini au ukanda anaotoka, anaathirika pia.
Ndio maana tunawakumbusha Watanzania kwamba uchaguzi umekwisha. Kilicho mbele sasa ni tudumisheni amani na umoja ili kujenga nchi. Mungu Ibariki Tanzania!.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni